
Utangulizi:
Mchungaji Dkt. Eliona Isaac Kimaro ni mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, na kwa sasa ni Mchungaji kiongozi katika Usharika wa Kijitonyama. Kwa zaidi ya miaka 30 sasa , Mchungaji Kimaro amejitolea kumtumikia Mungu kwa nafasi mbalimbali ndani na nje ya kanisa, akiwa mhubiri na Mwalimu wa Neno la Mungu hasa akijikita katika falsafa ya uchumi KIBIBLIA.
Maisha ya Awali ,Elimu na Biashara:
Mchungaji Dkt.Eliona Kimaro alizaliwa 25 September 1975 katika Kijiji cha Kondeni Matala, Marangu Mkoa wa Kilimanjaro. Mchungaji Kimaro alikulia katika mazingira ya kijijini ambako alipata malezi ya kidini na maadili mema. Tangu akiwa mtoto mdogo, alionyesha upendo mkubwa kwa huduma ya kanisa na aliitwa “Mchungaji” na wenzake kutokana na bidii yake ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kanisa. Tangu utotoni mwake aliendelea kushikilia wito wake wa huduma, mpaka ndoto yake ya kuwa Mchungaji ilipotimia.
Huduma ya Kichungaji
Mchungaji Dkt.Eliona Kimaro katika huduma yake ya kichungaji amelea watu wengi kiroho katika sharika na maeneo mbalimbali. Tangu mwaka 1990 alipoanza kama Mwinjilisti na Mhubiri wa neno la Mungu huko usharika wa Kana Tanga, mpaka mwaka 2005 alipojiunga na chuo cha Stephano Moshi Memorial University, Kampasi ya Theolojia Mwika na baadae kubarikiwa rasmi kuwa Mchungaji wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani tarehe 6 September 2009.
Kwa mara ya kwanza kabisa alianza kuhudumu kama Mchungaji katika Usharika wa Kariakoo, ambapo hapo ndipo Mchungaji Dkt.Eliona Kimaro, aliasisi ibada za masifu ya asubuhi (Morning Glory) na pia kuanza kurusha ibada kupitia mtandao wa Youtube, hivyo mataifa yote duniani yakaanza kushiriki ibada hizo, na mpaka sasa sharika nyingi za Kilutheri zinatumia utaratibu huu. Mwaka 2016 Mchungaji Dkt.Eliona Kimaro aliasisi Upendo TV kwa kusaidia kupatikana mitambo yake yenye thamani ya zaidi ya Shillingi Million 200 kwa wakati huo, na kituo hiki kilianza kufanya kazi rasmi na kuzinduliwa mwaka 2017 pale usharika wa KKKT Kijitonyama na mpaka sasa kituo hiki cha habari cha Kanisa kinafanya vizuri sana.
Akiwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kariakoo, pia alifanikiwa kununua shamba la hekari 120 huko chasimba Bagamoyo, na kuanzisha ujenzi wa kituo cha faragha na maombi kilichopewa jina la Bethel Retreat Centre. Akiwa na maono ya kutengeneza kituo kikubwa Zaidi cha faragha na maombi barani Afrika, kinachomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Mungu aliendelea kumtumia Mchungaji katika mambo mbalimbali na baadae mwaka 2017 alihamishiwa usharika wa kijitonyama, ambako Mungu ameendelea kumtumia kuponya Maisha ya watu mbalimbali mpaka sasa.
Katika huduma yake ya Kichungaji pia Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro amekutana na changamoto kadhaa, ikiwemo kusimamishwa huduma ya kichungaji mara mbili. Mara ya kwanza alisimamishwa miezi mitano akiwa usharika wa Kariakoo, na Mwaka 2023 alisimamishwa kwa muda wa siku 60 akiwa Mchungaji Kiongozi wa usharika wa Kijitonyama. Tukio hili la kusimamishwa kwa siku 60 lilileta hisia tofauti miongoni mwa waumini wa madhehebu yote ya kikristo na mpaka dini zingine, na kupeleka mpaka wengine kumuweka katika mabango barabarani (billboards) na vyombo mbalimbali vya habari viliandika kuhusu sakata hili. Kwa Neema ya Mungu lilimalizika , na Mchungaji Kimaro alirejea kazini. Katika kipindi hiki alichokua amesimamishwa, Usharika wa Kijitonyama ulipitia misukosuko kadhaa, ikiwemo maandamano ya washarika, na watu kutokuhudhuria ibada kama ilivyozoeleka.
Baada ya kurejeshwa kazini mnamo 17 March, alienda kufanya ibada ya shukrani katika usharika wake wa nyumbani, ambako ndiko alikobatizwa, usharika wa Kondeni Matala. Kupitia Ibada hiyo ya Shukrani, iliyofanyika tarehe 23 April 2023, Mchungaji Kimaro akisindikizwa na Rafiki zake, waliweza kuchangia Zaidi ya Shilingi milioni 400, ambazo zimetumika katika kumaliza ujenzi wa kanisa hilo la Kondeni Matala, huko Dayosisi ya kaskazini. Si hivyo tu, kupitia ibada hiyo lilizaliwa wazo la kumzawadia aliekua Mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa wakati huo, Askofu Dkt.Fredrick Onaeli Shoo, gari binafsi la kutembelea. Hivyo Mchungaji Kimaro pamoja na marafiki walimkabidhi rasmi Askofu Dr.Fredrick Shoo gari aina ya Toyota Land Cruiser GR Sport ya mwaka 2023 yenye thamani ya Zaidi ya shilingi Milioni 500, siku ya tarehe 23 September 2023, Nyumbani kwake Maili Sita, Moshi.
Mchungaji Kimaro ameendelea kuwa baraka hata katika makanisa mengine. Mnamo Tarehe 19 Novemba 2023, aliongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Anglican, St.James Arusha. Katika Ibada hii kwa Neema ya Mungu, walifanikiwa kuchangisha Zaidi ya Shilingi milioni 300 za kitanzania.
Si hivyo tu, pia Mchungaji Dkt.Eliona Kimaro ameendelea kuhudumu na kuwa baraka hata katika mambo makubwa ya kitaifa. Kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo amekua akialikwa kama mtoa mada katika kongamano la kitaifa la kodi na uwekezaji linaloandaliwa na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amealikwa katiks taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali,kutoa mada na mafunzo kuhusu maadili na uzalishaji na kuchangia mabadiliko chanya ya kiutendaji katika taasisi hizo.
Mungu ameendelea kumtumia sana Mchungaji Dkt.Eliona Kimaro kugusa Maisha ya watu mbalimbali, na ameendelea kumtumia kwa viwango vikubwa Zaidi katika kulipeleka mbele kanisa na kazi ya Mungu kiujumla.
Msururu wa Madigrii ya Mchungaji Kimaro:
Maisha aliyotokea Mchungaji Kimaro yalikua ni ya hali duni sana na yaliyojaa changamoto nyingi. Hali hii ilisababisha yeye kukosa ada ya kulipa masomo ya sekondari na kushindwa kusoma na kukaa nyumbani kwa miaka miwili baada ya kumaliza darasa la saba pamoja na kuwa alifaulu sana. Hata ilipotokea nafasi ya yeye kwenda kusoma Tanga, Mama yake alikosa fedha kabisa za kumpatia, na alimpa majani ya kahawa akiyatemea temea mate na kumuombea akimwambia “Mungu atakwenda kugeuza majani haya ya kahawa kuwa fedha huko unakokwenda, ningekua na uwezo ningekupa fedha za kukusomesha kama wazazi wengine walivyo na uwezo wa kutoa fedha za ada za Watoto. Lakini mimi sina uwezo, uwezo wangu nilionao ni haya majani ya kahawa. Ninayachuma kutoka kwenye mti huu, ninayatemea mate, nenda mwanangu ukasome, Mungu atayageuza majani haya kuwa fedha na utaenda kusoma. Nenda ukasome na usiache kwenda kusoma”. Kwa sababu hii, Mchungaji Kimaro aliweka nadhiri kuwa ikiwa yeye amekosa ada na kushindwa kusoma, basi Mungu akimbariki na akampa anuani, atahakikisha vijana wengine ambao watakua na changamoto kama zake za kukosa ada na kuishi kwenye umaskini uliokithiri basi yeye atawagharamia kuwasomesha ili wasije shindwa kusoma kwa sababu tu ya kukosa fedha
Kwa nadhiri hiyo aliyojiwekea, Kwa zaidi ya miaka 10 sasa Mchungaji Kimaro amesomesha zaidi ya vijana 200 katika ngazi mbalimbali za elimu, kuanzia sekondari hadi shahada za uzamivu. Mpaka hivi sasa vijana Zaidi ya 180 wana Bachelor Degree (Shahada ya kwanza), Zaidi ya 20 wana Master’s Degree (Shahada Uzamili) na 4 wana PhD (Shahada ya Uzamivu). Vijana aliowasomesha wamefanikiwa kuweza kuwa katika fani mbalimbali, wengine wamekua mapadri, madaktari, wachungaji, wainjilisti, wafanyabiashara wahandisi, wanahabari, wanasheria, marubani na fani nyinginezo nyingi
Kwa huduma yake hii ya kujitoa na kusomesha vijana wanaopitia katika mazingira magumu, kwa miaka tofauti ametunukiwa shahada tatu za uzamivu za heshima kutoka taasisi mbalimbali za elimu. Shahada hizo ni Shahada ya Uzamivu ya Utu (Honorary Doctorate in Humanitarian) kutoka nchini Zimbabwe, Shahada ya Uzamivu ya Divinity (Honorary Doctorate in Divinity) kutoka Los Angeles Marekani, na Shahada ya Uzamivu ya Uchumi KIBIBLIA (Honorary Degree in Religious Economics) kutoka California Marekani, hivyo sasa anatambulika kama Mchungaji Dkt.Eliona Isaac Kimaro
Ubunifu katika Huduma:
Mchungaji Kimaro amekuwa mstari wa mbele katika ubunifu wa huduma za kanisa, akianzisha huduma za ibada za masifu ya asubuhi na jioni, (Morning Glory na Evening Glory) pamoja na ibada za kusifu na kuabudu (Jumapili ya Kwanza kila mwezi) ambazo zimeleta baraka na kuimarisha imani ya waumini wengi na sasa zimeanza kutumika katika sharika mbalimbali za KKKT kote nchini.
Yeye pia alikuwa mchungaji wa kwanza wa KKKT kuanzisha ibada mtandaoni kupitia YouTube, na sasa sharika nyingi za dayosisi yake na dayosisi zingine zinafuata mfumo huu ili kuwafikia watu wengi zaidi. Huduma hii ya ibada mtandaoni imeweza kugusa maisha ya watu wengi, ndani na nje ya nchi.
Hii imemfanya kuwa mchungaji wa kwanza wa KKKT kutumia TEHAMA, na Mitandao ya kijamii kueneza Injili, kitu ambacho mwanzoni kilionekana ni kinyume cha utaratibu na utamaduni wa KKKT.
Hakuishia hapo, Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro pia aliasisi matumizi ya screen/Luninga kubwa kanisani, ambayo huwawezesha washarika hata walioko nje kuona vizuri, lakini pia kupata kujifunza Neno la Mungu kwa ufanisi Zaidi, kwani Mhubiri huweza kutumia presentations mbalimbali katika mahubiri na watu wakaona kwa urahisi.
Mchungaji Kimaro, ameasisi utoaji wa sadaka ya Fungu la Kumi, ambayo haikua utaratibu wa kawaida katika makanisa ya KKKT. Lakini pia, aliasisi mfumo wa watu kutoa sadaka kwa njia ya mtandao, iliyotoa urahisi kwa watu wengi zaidi kushiriki katika ibada na kutoa sadaka kupitia mtandao.
Katika kuleta ufanisi zaidi katika ibada, Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro kwanza alianzisha “Praise Team” kwa ajili ya kuongoza vipindi vya kusifu na kuabudu katika ibada, lakini pia aliasisi mfumo wa kanisa kumiliki PA System, tofauti na awali ambapo kwaya ndio zilikua zikimiliki mifumo hiyo, na kusababisha kushuka kwa ufanisi wa ibada, inapotokea kwaya imesafiri.
Katika kuhakikisha anaufikia ulimwengu, Mchungaji Kimaro aliasisi kutoa mafundisho kwa wanafunzi wa kipaimara kwa njia ya mtandao, hii ililenga kuwafikia wakristo walioko ughaibuni na wanakosa huduma za kiroho kwa ajili ya Watoto wao.
Katika huduma yake ya kichungaji pia ameasisi huduma iitwayo “Big September” ambapo kwa mwezi mzima, Wachungaji mbalimbali hukusanyika na kutoa huduma za ushauri na utunzaji kichungaji pamoja na ushauri nasihi. Huduma hii imekua baraka kwa watu wengi ambao Mungu amewaponya majeraha katika mioyo yao, na pia imewasaidia wachungaji wengi kuleta mabadiliko kwenye sharika zao
Uandishi:
Mchungaji Kimaro ameandika vitabu viwili: “Kutoka Ndoto Mpaka Hatima” na “Kujitunza Nafsi”. Vitabu hivi vimekuwa msaada mkubwa kwa wasomaji wengi katika kukuza imani yao na kupata maarifa ya jinsi ya kujitunza kiroho na kimwili. Mafundisho yake yamewabariki watu wengi na kutoa mafunzo ya uchumi KIBIBLIA, ambayo yamewawezesha vijana wengi kupata uhuru wa kiuchumi katika kazi zao na maisha yao ya kila siku.
Mzigo kwa Vijana wa Afrika:
Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro ana mzigo mkubwa juu ya vijana wa Kiafrika. Anaamini kwamba vijana ni nguzo muhimu katika maendeleo ya bara la Afrika. Kwa hiyo, ameanzisha na kuendesha miradi mbalimbali inayolenga kuwasaidia vijana kumjua Mungu, kufanikiwa kielimu na kiuchumi, na kuwa msaada kwa jamii zao na Afrika kwa ujumla. Miradi hii ni pamoja na warsha za ujasiriamali, programu za elimu ya Biblia, program za mafunzo ya uchumi KIBIBLIA, program za malezi na program ya kutoa msaada wa kifedha kusomesha vijana wenye mahitaji maalum
Moja ya program hizo ni YOUTH OVERNIGHT (Usiku wa Vijana), ambapo huwa ni mkesha wenye kujumuisha wazungumzaji waliofanikiwa katika maeneo mbalimbali ya kimaisha kupata fursa ya kufanya majadiliano na vijana katika kuona ni namna gani wanaweza kupiga hatua. YOUTH OVERNIGHT hujumuisha mada kama Uchumi na Uwekezaji, Afya ya Akili, na Kutumia Vipaji kujiendeleza.
Si hapo tu, pia ameasisi program ya Vijana ijulikanayo kama YOUTH VISION CAMP ama MTOKO WA MCHUNGAJI NA VIJANA, ambayo hufanyika katika kambi maalum nje ya neo la usharika, ambapo vijana hupata nafasi ya kufanya tafakari binafsi ya kina, hupata nafasi ya kufanya maombi, kujifunza kwa mapana juu ya Uchumi KIBIBLIA, Uwekezaji, Nidhamu Binafsi na Afya ya Akili, huku wakipata nafasi ya kuwa pamoja na vijana wengine katika majadiliano ya kina pamoja na michezo. Kambi hizi zimekua msaada mkubwa kwa vijana zikiwafungua fikra na kuwapa mwanga wa kuanza kujiumba upya na kuwa bora zaidi.
Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro ni kiongozi wa kiroho mwenye maono, mwalimu wa neno la Mungu, anayeamini katika nguvu ya maarifa na uthubutu kwa ajili ya kuboresha maisha ya waumini wake na jamii kwa ujumla. Amejitoa kwa dhati katika huduma yake, na kazi yake inaendelea kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wengi.